WAZIRI NYANSAHO APONGEZA JKT NA JWTZ KWA KUIMARISHA ULINZI, ASEMA VINACHANGIA AJIRA NA MAENDELEO
Na Madina Mohamed
Dar es Salaam – Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amevipongeza viongozi na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa juhudi wanazozifanya katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
Dkt. Nyansaho ametoa pongezi hizo Julai 6, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema utendaji wa vyombo hivyo umeendelea kuwa msingi wa kudumisha amani na utulivu unaowapa wananchi fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema mazingira ya amani na usalama yanayolindwa na JKT na JWTZ yana mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwani wananchi wanaendelea kufanya shughuli za kiuchumi bila hofu.
Waziri huyo alieleza kuwa mbali na jukumu la ulinzi, JKT imeendelea kutekeleza shughuli za uzalishaji mali pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana, hatua inayowajengea uwezo wa kujitegemea na kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Aidha, amesema ushiriki wa JKT na JWTZ katika Maonesho ya Sabasaba umeziwezesha taasisi hizo kuonesha kwa wananchi shughuli mbalimbali wanazozitekeleza, ikiwemo utoaji wa huduma, uzalishaji mali, mafunzo kwa vijana na matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia mchango wa JKT katika ajira, Dkt. Nyansaho amesema kampuni ya usafi na unyunyuzi dawa ya SUMAJKT imefanikiwa kuajiri vijana 4,800, jambo linaloonesha namna taasisi hiyo inavyochangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuziimarisha taasisi za ulinzi na usalama ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, sambamba na kuendelea kutoa fursa kwa vijana kupitia mafunzo na shughuli za uzalishaji zinazochochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Comments
Post a Comment