WAZIRI KAPINGA AIPONGEZA TUME YA USHINDANI (FCC) KWA KAZI YA KUDHIBITI BIASHARA NA KULINDA WALAJI ‎



‎Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM JAMII HURU 

‎ Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amekiri juhudi kubwa zinazofanywa na Tume ya Ushindani (FCC) katika kudhibiti masoko, kulinda walaji, na kuhakikisha bidhaa feki hazingii sokoni. Waziri Kapinga alitoa pongezi hizo leo alipotembelea ofisi za FCC zilizopo jijini Dar es Salaam, akielezea namna tume hiyo inavyofanya kazi muhimu katika kuimarisha ushindani na ufanisi katika sekta ya biashara.

‎Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri Kapinga alisema kuwa moja ya majukumu makubwa ya FCC ni kuhakikisha kwamba usimamizi wa biashara unakuwa imara, na kwamba ni lazima kuhakikisha bidhaa zinazozunguka katika soko ni bora, salama na zinazokidhi viwango vinavyohitajika. Aliongeza kuwa tume hiyo pia inatoa elimu kwa watanzania kuhusu haki zao kama walaji na jinsi ya kutambua bidhaa feki.

‎“Watanzania wanatufahamu vizuri, na wao ndio walaji wetu. Kwa hiyo, tunapoongea kuhusu masuala ya biashara, tunapaswa kufikiria namna ya kutimiza matarajio ya walaji hawa. Kikao cha leo kimekuwa ni muhimu sana kwetu kwani tunajitahidi kutengeneza misingi madhubuti itakayoongeza ufanisi na kuhakikisha tunaleta manufaa makubwa kwa jamii na kwa biashara nchini,” alisema Waziri Kapinga.

‎Waziri Kapinga aliongeza kuwa lengo la ziara hiyo ni kutathmini na kuimarisha mifumo ya kazi ya FCC ili kuendana na mahitaji ya soko la sasa, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza njia bora za upatikanaji wa mrejesho kutoka kwa walaji na wadau wengine wa biashara.

‎Mikakati ya Kudhibiti Bidhaa Feki na Kuboresha Ushindani

‎Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga alisisitiza kuwa mikakati ya kudhibiti bidhaa feki itaendelea kuimarishwa kwa kuongeza mbinu za kisasa za ufuatiliaji wa soko, huku akielezea kuwa wamejizatiti kuboresha ubunifu na teknolojia ili kutoa huduma bora zaidi.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ushindani (FCC), Hadija Juma Ngasongwa, alisema kwamba kazi kubwa inayofanywa na FCC inalenga kufuata falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kukuza na kuimarisha biashara na uwekezaji nchini. Bi Kasongwa aliongeza kuwa FCC inahakikisha kwamba miunganiko ya makampuni na viwanda inafanyika kwa kuzingatia ushindani wa haki, hivyo kutoa fursa kwa makampuni makubwa na madogo kuendana kwa faida ya uchumi wa taifa.

‎“Kwa miaka minne sasa, tunashughulikia miamala ya miunganiko ya makampuni na kuchambua mikataba hiyo kwa lengo la kuongeza mitaji na kuokoa ajira. Tume imetenga mbinu mpya za kuhimiza ushindani, na kuhakikisha tunadhibiti bidhaa zisizokidhi viwango,” alisema Bi Ngasongwa.

‎Kurekodi Usafirishaji wa Bidhaa

‎Vile vile, Bi Ngasongwa alitangaza kuwa kuanzia Desemba 1, 2025, zoezi la kurekodi usafirishaji wa bidhaa zote zinazoingia nchini litaanza. Zoezi hili linatarajiwa kusaidia kufuatilia uingiaji wa bidhaa feki na zisizokidhi viwango, na hivyo kuboresha utendaji wa sekta ya biashara kwa ujumla.

‎“Zoezi hili la kurekodi usafirishaji linalenga kudhibiti bidhaa zisizofaa kabla ya kuingia sokoni. Lengo letu ni kulinda maslahi ya walaji, kuimarisha usalama wa bidhaa na kuzuia udanganyifu katika soko,” aliongeza.







Comments

Popular posts from this blog

IDD AZZAN AJA KIVINGINE TENA JIMBO LA KINONDONI

WANAOSEMEKANA KUWA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA*

DOLA MILIONI 2 ZA KIMAREKANI Kununufaisha WAKULIMA NCHINI