MBETO:HAMZA HASSAN HANA MPINZANI JIMBO LA SHAURIMOYO




‎Na Madina Mohammed ZANZIBAR 

‎Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, leo amezindua rasmi kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mji wa Zanzibar Magharibi, ndani ya Jimbo la Shaurimoyo, katika harakati za kuimarisha nafasi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa hivi karibuni.

‎Mbeto aliongoza uzinduzi huo akimnadi Mbunge wa sasa wa Shaurimoyo, Hamza Hassan, pamoja na madiwani wa kata zote zilizopo katika jimbo hilo. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mbeto alieleza kwa furaha kwamba Hamza Hassan ameonyesha umahiri mkubwa katika utendaji kazi wake akiwa mbunge, na kwamba amekuwa ni mchapakazi mwenye dhamira ya dhati ya kutumikia wananchi wa Jimbo la Shaurimoyo.

‎“Hamza Hassan amekuwa akifanya kazi kubwa, si tu kama Mbunge bali pia kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar. Kazi zake zinajulikana, miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa chini ya uongozi wake. Tunajivunia kuwa na kiongozi kama yeye, ambaye amewezesha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali. Hakuna sekta ya wizara yoyote ambayo inamwambia Hamza anashindwa kazi, yeye ni mtaalamu wa kazi zote,” alisema Mbeto huku akiwahamasisha wananchi kuendelea kumchagua kwa kishindo.

‎Mbeto pia alitaja mafanikio ya serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dr. Hussein Ali Mwinyi, akisisitiza kuwa miradi ya maendeleo katika jimbo la Shaurimoyo ni dhihirisho la kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali. Alisema kuwa hakutarajia kuona kura yoyote ikipotea kwa upande wa CCM kwenye uchaguzi huu.

‎Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shaurimoyo,Hamza Hassan, alizungumza kwa hisia kubwa akielezea mafanikio ambayo yamepatikana kwa ushirikiano na wananchi wake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Aliwahakikishia wananchi kuwa ahadi nyingi zilizotolewa zimeanza kutekelezwa na nyingine ziko njiani kutekelezwa, hasa katika masuala ya miundombinu na maendeleo ya kijamii.

‎“Katika kipindi kilichopita, tumeshirikiana sana na wananchi wetu katika kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi. Moja ya ahadi yetu kubwa ilikuwa ni kuleta maendeleo ya barabara katika maeneo yetu. Barabara ya Mboriborini, ambayo kwa miaka mingi ilikuwa katika hali mbaya, sasa inajengwa na ninyi ni mashahidi wa maendeleo hayo,” alisema Hamza.

‎Akiendelea, Hamza alitaja miradi mingine inayotekelezwa katika jimbo lake, akiwemo mradi wa barabara inayotoka Mchumbani na kuunganisha hadi Uwanja wa Kihuni, ambayo itaanza kujengwa hivi karibuni. Alisema kwamba kwa sasa, mkandarasi tayari amepatikana na ujenzi utaanza haraka.

‎"Kuna pia maombi ya kiwanja cha Urafiki, ambapo tumeomba kwa Rais ili kiwanja hicho kijengwe na kuwa cha kisasa kama viwanja vingine vya michezo. Tunaendelea kuimarisha miundombinu ya kijamii kwa manufaa ya wananchi wetu,” aliongeza Hamza.

‎Mhe. Hamza pia alizungumzia mipango ya ujenzi wa viwanja vya kisasa katika maeneo ya Shaurimoyo, akitoa mfano wa viwanja vya Kihumbi na Mboriborini, ambavyo tayari wataalamu wamefika na kupima. Aliwahimiza wananchi, hasa waishio jirani na maeneo hayo, kutoa ushirikiano ili kupanua maeneo ya viwanja na kujenga majengo ya ghorofa.

‎“Ningependa kuwasihi majirani wa maeneo haya kufikiria mustakabali wa maendeleo yetu na kutoa nafasi kwa ujenzi wa majukwaa ya michezo na nyumba za ghorofa. Hii itasaidia kuboresha mazingira yetu na kutoa fursa kwa familia kupata makazi bora,” alisisitiza Hamza.




Comments

Popular posts from this blog

IDD AZZAN AJA KIVINGINE TENA JIMBO LA KINONDONI

WANAOSEMEKANA KUWA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA*

DOLA MILIONI 2 ZA KIMAREKANI Kununufaisha WAKULIMA NCHINI