‎MRISHO KAMBA AAHIDI MAGEUZI MAKUBWA SANDALI, AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KUANZA KAMPENI ‎



‎Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM JAMII HURU 

‎Dar es Salaam, Agosti 27, 2025 — Mgombea Udiwani wa Kata ya Sandali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mrisho Kamba, amesema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa kata hiyo na ameahidi kuleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo iwapo atachaguliwa kuwa diwani.

‎Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurudisha barua ya uteuzi kutoka ofisi za Kata ya Sandali, Kamba alisema amefarijika sana na imani ambayo chama chake kimemuonesha kwa kumpa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo muhimu ya uongozi.

‎"Nimepokea kwa moyo wa shukrani uteuzi huu kutoka CCM. Ni heshima kubwa na wajibu mzito ambao nipo tayari kuubeba kwa ajili ya maendeleo ya Sandali na ustawi wa wananchi wake," alisema Kamba.

‎Kamba alieleza kuwa ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha kata ya Sandali inapiga hatua kimaendeleo kupitia mipango ya kimkakati katika sekta za elimu, afya, miundombinu na uwezeshaji wa vijana na wanawake kiuchumi.

‎Aidha, aliwataka wananchi wa Kata ya Sandali kujitokeza kwa wingi kesho Agosti 28, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM. Alisisitiza umuhimu wa kuwaunga mkono viongozi wa juu wa chama hicho akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wa urais Dkt. Emmanuel Nchimbi.

‎"Ni wakati wa kuonesha mshikamano wetu. Tuoneshe kuwa Sandali iko pamoja na CCM, tuko pamoja na Mhe. Rais Samia na Dkt. Nchimbi kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu," aliongeza.

‎Udiwani wa Kata ya Sandali ni nafasi yenye ushindani mkubwa, lakini Kamba amesema anajivunia kuwa na uzoefu, maono na uhusiano mzuri na wananchi wa kata hiyo, hali inayompa matumaini makubwa ya ushindi.

Comments

Popular posts from this blog

IDD AZZAN AJA KIVINGINE TENA JIMBO LA KINONDONI

WANAOSEMEKANA KUWA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA*

DOLA MILIONI 2 ZA KIMAREKANI Kununufaisha WAKULIMA NCHINI