SAMIA NETBALL CUP 2025 YAZINDULIWA RASMI: ZAWADI NONO KUMNUFAISHA MWANAMKE KUPITIA MICHEZO

 


Dar es Salaam, 27 Julai 2025 –

 Mashindano ya mpira wa netball kwa Mkoa wa Dar es Salaam, yanayojulikana kama Samia Netball Cup 2025, yamezinduliwa rasmi leo, kwa lengo la kutoa fursa kwa wanawake na mabinti kushiriki katika michezo ya netball huku wakijenga afya zao na kujiimarisha kiuchumi. Hafla hiyo ilifanyika kwenye viwanja vya Twende Pamoja na Mama Spoti Promotion, ambapo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali na mashabiki wa michezo.

‎Akizungumza na Habari Leo, mwandaaji wa mashindano hayo na Mtendaji Mkuu wa Twende Pamoja na Mama Spoti Promotion, Kasimu Ahmad, alieleza kuwa lengo kuu la mashindano haya ni kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kujitokeza na kuonesha vipaji vyao katika michezo ya netball.

‎“Kumekuwa na michezo mingi, lakini kwa sasa tumeona ni muhimu kuanzisha mashindano ya netball kwa wanawake kwani wanastahili jukwaa la kuonesha vipaji vyao. Huu ni mchango wetu katika kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake za kuinua wanawake kupitia michezo,” alisema Kasimu.

‎Mashindano ya Samia Netball Cup 2025 yanajivunia zawadi nono kwa washindi, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa wanawake wanapata motisha na maendeleo kupitia michezo. Mshindi wa kwanza atazawadiwa Shilingi Milioni 5, kombe, na medali, huku mshindi wa pili akipata Shilingi Milioni 3 na medali. Mshindi wa tatu atajinyakulia Shilingi Milioni 1 na laki tano, na mshindi wa nne atapata Shilingi laki tano. Aidha, mfungaji bora atapewa Shilingi laki mbili, na kikundi bora cha hamasa kitaondoka na zawadi maalum kama njia ya kutambua mchango wao katika kuhamasisha mashabiki na timu.



‎“Kwa upande wetu, mashindano haya ni fursa kubwa kwa wanawake kujiajiri na pia kujiimarisha kiuchumi. Tunategemea kuona wanawake wengi wakitumia fursa hizi kupata maendeleo katika michezo na hata katika maisha yao ya kila siku,” aliongeza Kasimu.

‎Nahodha wa timu ya Konfoti, Prisca Godlove, alitoa shukrani kwa serikali ya Rais Samia kwa kutunga na kuendesha mashindano haya ambayo yanatoa jukwaa kwa wanawake kushiriki katika michezo na kujitangaza.

‎“Tunaishukuru serikali kupitia Rais Samia kwa kuona umuhimu wa wanawake katika michezo. Sisi kama wachezaji tunajiandaa kuchangia kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha tunanufaika na fursa hizi. Hii ni fursa ya kujiajiri na kujiinua kimaisha kupitia michezo,” alisema Prisca.



‎Mchezaji kutoka timu ya Ulipo Tupo, Magreth Elia, alitoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuutangaza mchezo wa netball ili kuvutia watoto wa kike, hususani katika maeneo ya mijini na vijijini.

‎“Vyombo vya habari vinapaswa kuendelea kutoa nafasi ya kutangaza mchezo wa netball ili watoto wa kike wawe na mifano ya kuigwa. Tunahitaji kuona michezo hii ikikua zaidi, na zaidi ya yote, kuwa na vipaji vya wanawake vinavyoibuka na kuleta mabadiliko,” alisema Magreth.

‎Mashindano ya Samia Netball Cup 2025 yamepambwa na burudani, maonyesho, na maandalizi ya kuvutia, yakilenga kuwa na mabadiliko makubwa katika kuibua vipaji vya wanawake kupitia michezo. Kauli mbiu ya mashindano hayo ni: “Michezo ni Ufunguo wa Maendeleo ya Mwanamke na Taifa.”

‎Hafla ya uzinduzi wa mashindano haya imeibua matumaini makubwa miongoni mwa wanawake na mabinti wa Mkoa wa Dar es Salaam, huku wengi wakijivunia fursa hii ya kuonesha vipaji vyao na kuchangia maendeleo ya michezo nchini.

Comments

Popular posts from this blog

IDD AZZAN AJA KIVINGINE TENA JIMBO LA KINONDONI

WANAOSEMEKANA KUWA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA*

DOLA MILIONI 2 ZA KIMAREKANI Kununufaisha WAKULIMA NCHINI