MGOMBEA UBUNGE SIKONGE AKUMBWA NA SKENDO NZITO
Wakati vuguvugu la mchujo wa wagombea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) likizidi kupamba moto, mgombea ubunge wa Jimbo la Sikonge, Samwel Mchele Chitalilo, amejikuta katika hali ngumu baada ya kufichuliwa kwa tuhuma nzito kuhusu mienendo yake, zilizotolewa na watu wa karibu.
Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa watu wa karibu wa Chitalilo—ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe—alisema kuwa moja ya makosa makubwa ambayo wananchi wa Sikonge wanaweza kufanya ni kumpitisha Chitalilo kuwa mbunge, kwani hana sifa wala maadili yanayostahili kiongozi wa umma.
“Huyu jamaa msimuone tu anavyotabasamu; sisi tuliomzoea tunamjua vizuri. Nimeamua kusema ukweli kwa sababu dhamira yangu hainiruhusu kunyamaza. Chitalilo ana tabia nyingi zisizofaa, ikiwemo kuchukua wake za watu bila haya, eti kwa sababu ana pesa! Amewaumiza watu wengi sana. Na suala la utapeli bado lipo—hilo halijawahi kuisha,” alieleza.
Aliongeza kuwa kipindi akiwa mbunge aliwahi kumtapeli mamilioni ya fedha mfanyabiashara mmoja aitwaye Bwana Athuman Kaponola, lakini kutokana na ushawishi wake wa kisiasa wakati huo, suala hilo lilifunikwa kimyakimya. “Sasa amerudi tena kwa gia mpya kutaka ubunge. Nawahurumia wananchi watakaomchagua. Tunaomba CCM isimpe nafasi watu wa aina hii kugombea uongozi,” alisema.
Chitalilo aliwahi kukumbwa na kashfa ya kutuhumiwa kumtapeli Kaponola zaidi ya shilingi milioni 100—sakata ambalo liliwasilishwa hadi Ofisi ya Bunge jijini Dodoma na pia kufikishwa kwa Waziri Mkuu.
Katika tuhuma hizo, Kaponola anadai kuwa mwaka 2008, Chitalilo alimshawishi kuingia ubia wa biashara ya kuagiza na kuuza pikipiki aina ya Dayun, pamoja na matairi na mipira ya ndani kutoka China, kupitia kampuni ya Oceanic Distributors Ltd, ambayo inaelezwa kumilikiwa na mbunge huyo.
Chitalilo alikiri kuwepo kwa madai hayo, lakini alisisitiza kuwa deni hilo linaihusu kampuni yake binafsi na si yeye kama mtu.

Comments
Post a Comment