TFS YAWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA DUNIA KUHUSU MABADILIKO YA TABIANCHI
Na Mwandishi Wetu – Bonn
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa 62 wa utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (SBI & SBSTA 62), uliofanyika jijini Bonn, Ujerumani, kuanzia tarehe 16 hadi 26 Juni, 2025.
Mkutano huo wa kimataifa ulihusisha majadiliano ya kitaalamu kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris, ukilenga kuweka mikakati ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto, kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuharakisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya TFS, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TFS, SACC Dkt. Zainabu Bungwa, alisisitiza kuwa shughuli za uhifadhi wa misitu zinazofanywa na TFS zina nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.
“Mikakati ya TFS katika kuhifadhi na kuendeleza misitu ya asili na ya kupandwa ni nyenzo ya msingi katika kupunguza gesi joto, kuhifadhi vyanzo vya maji, na kuongeza ustahimilivu wa jamii zinazozunguka misitu dhidi ya athari za tabianchi,” alisema Dkt. Bungwa.
Mkutano huo ulijadili kwa kina agenda za kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa nchi wanachama kuhakikisha miradi ya biashara ya kaboni (carbon markets) inasajiliwa, kufuatia kukamilika kwa mifumo ya kitaifa na kimataifa ya usimamizi wa biashara hiyo.
Aidha, mijadala ilihusu pia uhuishaji wa mifuko ya kifedha ya mazingira kama Green Climate Fund (GCF), Global Environment Facility (GEF), Adaptation Fund (AF) na Special Climate Fund (SCF), pamoja na kuanzishwa kwa mfuko mpya wa fidia ya hasara na maafa (Loss and Damage Fund).
Vikao hivyo pia vilijadili jinsi ya kusimamia mabadiliko ya haki (Just Transition), kama vile matumizi ya nishati safi ya kupikia na miundombinu ya usafiri wa haraka, ikiwemo reli ya kisasa (SGR), sambamba na maendeleo ya teknolojia rafiki na biashara zisizo na madhara makubwa kwa mazingira.
Mambo mengine yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na ushirikishwaji wa wanawake, vijana, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika juhudi za kimataifa za kukabili tabianchi.
Katika mkutano huo, TFS pia ilishiriki vikao mbalimbali vilivyoratibiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), ambapo ilibainisha dhamira yake ya kuendeleza ushiriki wa kitaifa katika utekelezaji wa malengo ya tabianchi kupitia uhifadhi wa misitu.
Kwa mujibu wa Dkt. Bungwa, TFS iko tayari kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha kuwa sekta ya misitu inatumika kikamilifu kama injini ya kushughulikia changamoto za tabianchi na kukuza uchumi wa kijani.
“Misitu yetu si tu hazina ya maliasili, bali ni nguzo ya uhai wa Taifa. Tunahitaji kuiweka kwenye ramani ya kitaifa na kimataifa ya uwekezaji, biashara ya kaboni, na maendeleo endelevu,” alisisitiza.


Comments
Post a Comment