TUSIKUBALI KUCHONGANISHWA NA WACHACHE WENYE MASLAHI BINAFSI- MWIGULU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiwa kwenye Ziara yake ya Kikazi Mkoani Arusha, amesisitiza umuhimu wa kulinda amani kwa maendeleo na ustawi wa Watanzania, akiwataka wananchi kuamka na kuwakataa wale wote wanaowachonganisha kwa maslahi yao binafsi. Akieleza kuwafahamu baadhi ya Watanzania wanaolipwa fedha ili kuwagombanisha na kuwataka kuingia barabarani kufanya vurugu, Mhe. Nchemba ameeleza kuwa wanaohamasisha vurugu nchini wamekuwa na visingizio kadhaa vya kuwahadaa wananchi huku lengo lao likiwa ni kuwagombanisha watanzania ili kutaka kuzifaidi rasilimali za nchi. "Zimetokea vurugu, kwa aina ya vurugu zilivyotokea, kwanini hatushtuki? Wanatumia visingizio vingine lakini hapa kuna mchezo. Zimetolewa fedha wakapewa vijana na wale Vijana wakaandaa Vijana wenzao na kuwataka kufanya vurugu. Leo tujiulize wale wanaotoa hizo fedha watazirudishaje? Na kama ni maandamano, Kiongozi wake alikuwa nani? Waliandamana kutoka wapi kwenda wapi? ...